Rais Obama amehimiza kuwe na utulivu
Maafisa wa polisi huko Marekani walirusha mabomu ya machozi ili kutawanya halaiki ya watu waliokuwa wakiandamana , kwa usiku mwingine, katika mji wa Ferguson, jimbo la Missouri kupinga mauaji ya kijana mweusi.
Maandamano yalitibuka saa chache baada ya hotuba ya Rais Obama akisihi raia kuwa watulivu.
Chanzo cha maandamano hayo ni kuuawa kwa kijana mmoja mweusi, aliyepigwa risasi na maafisa wa polisi tarehe 9, mwezi huu.
Michael Brown, ambaye hakuwa na silaha yoyote, alipigwa risasi mara sita na polisi waliomshuku kuwa alikuwa ametekeleza wizi wa kimabavu katika duka moja mjini Ferguson.
Mwanasheria mkuu wa Marekani anatarajiwa kuzuru mji wa Ferguson atakapokutana na maafisa wanaopeleleza mauaji hayo.
Gavana wa Missouri Jay Nixon aliidhinisha kutumika kwa kitengo maalum cha polisi wa kuzima ghasia waliotumwa eneo hilo hapo jana ili kusaidia juhudi za polisi kurejesha amani, huku amri ya kutoruhusiwa kutoka nje iliyotangaza mwishoni mwa wiki iliyopita ikiondolewa.
Kuuwawa kwa Brown na askari mzungu kulizusha wasiwasi kati ya watu wa rangi tofauti katika eneo hilo, Ferguson, lililo na jamii yenye wakazi wengi weusi.
Afisa wa polisi Darren Wilson alimpiga risasi Michael Brown juma lililopita baada ya kumsimamisha kwa kutembea barabarani, kulingana na ripoti zilizotolewa.
Afisa mkuu wa polisi Ron Johnson, anayeendesha operesheni hiyo ya Ferguson, alisema maafisa wa polisi walilazimika kuingia mjini humo siku ya Jumanne, baada ya waandamanaji kuwashambulia kwa bunduki na kuwarushia mabomu ya petrol na machupa huku watu wawili wakipata majeraha ya risasi.
Alisihi waandamanaji kufanya maandamano yao nyakati za mchana ili kuzuia “baadhi ya wahalifu” kuanzisha vurugu kimakusudi.
"Yeyote ambaye amewahi kushiriki katika maandamano kama haya anafahamu kuwa kuna hatari nyakati za usiku: maandamano ya usiku huruhusu wahalifu wachache kujificha miongoni mwa halaiki ya watu na kujaribu kuleta vurugu,” Jonson alisema.
Maafisa wa polisi wakiwakamata waandamanaji Ferguson
Maafisa wa usalama pia waliamuru wanahabari kuondoka baada ya waandamanaji walikataa kutoa vizuizi barabarani.
Ushahidi wa video unaonyesha maafisa wa polisi wakiwakamata waandamanaji kadhaa, huku msururu wa maafisa wa polisi waliojihami wakiingia kukabiliana na umati wa watu waliojawa na hasira.