Timu ya Kenya ya voliboli ya wanawake ndio mabingwa wa mwaka huu wa mashindano ya Grand Prix.
Kenya
imesajili ushindi mkubwa wa seti 3-1 dhidi ya Peru katika fainali ya
mashindano ya voliboli ya wanawake ya Grand Prix kundi la tatu mjini
Canberra, Australia Jumapili.Kenya ilisajili ushindi wa alama 21-25, 25-17,25-22 na kisha 25-23.
Kufuatia ushindi huo Kenya ndiyo nchi ya kwanza ya Afrika kushinda taji la Grand Prix, ushindi ambao sasa umewapandisha kidada hao Malkia hadi kundi la pili.
Kwa upande wa Peru Levvy Angela aliongoza na pointi 26.
Mamia ya Wakenya wanaoishi Australia wakiongozwa na balozi wa Kenya nchini humo Isaiah Kabira waliwashangilia warembo hao wa Kenya waliovalia mavazi ya kuvutia ya rangi nyeupe na kijani kibichi.
Huku wachezaji wa Kenya wakidondokwa na machozi ya furaha, Peru nao waliambulia kilio cha kuchapwa na mabingwa wa Afrika kwani waliingia uwanjani na matumaini makubwa ya ushindi ikikumbukwa kwamba walishinda Kenya katika raundi ya kwanza nchini Mexico.
''Huu ndio mwanzo wa matokeo mengine bora zaidi katika mashindano ya dunia,'' anasema nahodha wa Kenya Praxidis Agala
''Tunashukuru Wakenya wanaoishi hapa kwa kutushangilia kuanzia mwanzo hadi mwisho.''
''Tuko tayari kupambana na miamba ya dunia.''
''Tulitizama kwa makini kanda za mechi za Peru walizocheza na tukapata mbinu ya kuwabana''.
Kenya ilishiriki kwa mara ya kwanza katika mashindano ya Grand Prix mwaka jana na kumaliza nafasi ya tano katika kundi la tatu.
Kulingana na mwenyekiti wa shirikisho la voliboli nchini Kenya, Waithaka Kioni, timu ya Kenya huenda ikarudi nyumbani Jumanne usiku.
Kioni ameiomba serikali itoe fedha za kuwawezesha kufanya mazoezi ng'ambo kabla wasafiri kwa kombe la dunia na michezo ya mataifa ya Afrika.
No comments:
Post a Comment