Sepp Blatter ameutingisha ulimwengu wa soka hapo jana kwa
kusema kwamba anajiuzulu akiwa kama Rais wa Shirikisho la Sola la
Kimataifa FIFA kutokana na uchunguzi wa rushwa ambao hivi sasa
unamjumuisha hata kiongozi huyo mwenyewe binafsi mwenye umri wa miaka
79. Mtu aliezungumza kwa sharti la kutotajwa jina ameliambia shirika la
habari la Uingereza Reuters hapo jana kwamba Blatter ambaye ameliongoza
shirika hilo linalosimamia soka duniani tokea mwaka 1998 anachunguzwa na
waendesha mashtaka wa Marekani na shirika la upepelezi nchini humo FBI.
Msemaji wa FBI amekataa kulizungumzia suala hilo.Blatter raia wa Uswisi
ambaye alikuwa ni mtu mwenye ushawishi mkubwa kwenye FIFA kwa miongo
mingi ametangaza uamuzi wake wa kujiuzulu katika mkutano na waandishi wa
habari ulioitishwa kwa haraka mjini Zurich hapo jana ikiwa ni siku sita
baada ya polisi kuivamia hoteli moja mjini humo na kuwakamata maafisa
kadhaa wa FIFA na ni siku nne baada ya kuchaguliwa tena kwa muhula wa
tano akiwa rais wa FIFA. Amesema uchaguzi wa rais mpya wa FIFA
utafanyika karibuni kadri inayowezekana lakini afisa mmoja wa FIFA
amesema iwapo uchaguzi huo utafanyika mapema basi itakuwa mwezi wa
Disemba.
No comments:
Post a Comment