Tuesday, 25 September 2018

MUPE,MURUKEE,MUPEE,MURUKEEE,MURUKEEEE......!!!!!!



Luca Modric mchezaji bora wa mwaka wa FIFA
Wameamua kumpa,ni baada ya kumdhurumu tuzo yake ya msimu wa 2009/10,mwaka huu wameona aibu.
Labda walimruka kwa makusudi ili watengeneze ushindani wa Lionel Messi na Cristiano Ronaldo uliodumu kwa miaka kumi.

Alikuwa kwenye kiwango bora kabisa cha kuweza kutwaa tuzo ya mchezaji bora wa dunia,lakini kwa kuwa jina lake lilikuwa haliuzi kutokana na klabu na ligi aliyokuwa akiichezea kwa wakati huo,wakaamua kumnyima kwa makusudi"a world is not fair at all"(dunia haina usawa kabisa).

Kitita cha Euro milion 15 (€15m) kilimng'oa Estadio Santiago Bernabeu na kuelekea Giuseppe Meazza kule jijini Milan kumpisha mfalme wa Rossoneri,aliyeacha alama kwenye dimba la San Siro,Ricardo Izecson Dos Santos Leite,Kakà.

Hakukawia kuingia kwenye mfumo wa Jose Mourinho.Nguvu ,stamina na nishati yake uwanjani vilimtofautisha na wachezaji wengi wa nafasi yake uwanjani,akiigawa mipira kwa staili anayoitaka yeye,yaan "mupe,murukee,mupee,murukee,murukee,mupeeee" kama muhudumu wa bar anayewahudumia wateja wake.
Ricardo Kaka mwanasoka bora duniani mwaka 2007

Wesley Benjamin Sneijder,mchezaji wa kimataifa wa Uholanzi aliyemnyima usingizi babu Sir Alex Ferguson wakati wa siku za neema za Manchester United,akiisaka sahihi yake usiku na mchana bila mafanikio.

Msimu wake wa kwanza kutua "Nerazzuri" ,aliisaidia Inter Milan kuchukua makombe makubwa matatu waliyoshiriki.Walichukua ubingwa wa ligi kuu nchini Italia "Serie A" maarufu kama Scudetto,walichukua kombe la Coppa Italia na kisha wakachukua ubingwa wa klabu bingwa barani Ulaya (UCL).

Katika nusu fainali ya klabu bingwa barani Ulaya,Inter Milan walikutana na mabingwa watetezi FC Barcelona,Sneijder aliwaonesha "Italian Job" viungo wa Barcelona waliounda sambusa yao iliyowekwa nta na Lionel Messi,Xavi Hernandez na Andres Iniesta huku Sergio Busquet akiishikilia vyema isianguke na kuingia mchanga.Matokeo ya jumla ya michezo yote miwili,Inter Milan aliingia fainali kwa jumla ya magoli 3-2.

Fainali ikapigwa Santiago Bernabeu,maskani ya pepo ya Sneijder iliyogeuka jehanamu kwake kutokana na ujio wa "Magalacticos " kama Cristiano Ronaldo na Ricardo Kaká.

Sneijder kama kawaida yake awapo uwanjani,akawa anatawanya mipira kuwalisha Diego Milito na Samuel Eto'o kwa mtindo ule ule wa MUPE,MURUKEE,MUPEE,MURUKEE,MURUKEE.Inter Milan wakawafunga Bayern Munich magoli 2-0 huku Sneijder akitoa "assist" moja kati ya magoli hayo yaliyofungwa na Diego Milito.

Wesley Sneijder licha ya kucheza kwenye kiwango cha juu sana hakuwahi kushinda tuzo

Sneijder akatua bondeni kwenye kombe la dunia,akaendeleza wimbi lake la kutawala eneo la kati,safari hii sio kuisaidia timu yake kufuzu kwa kushinda mechi zote nane za makundi,bali aliwapitisha salama kwenye bonde la uvuli na mauti ya soka kwa kuwafungia magoli matano kwenye michuano hiyo,mawili yakiwa dhidi ya "Selecao wa Brazil",na kumaliza mashindano wakiwa washindi wa pili na yeye kuwa na idadi sawa ya magoli na Thomas Müller,mfungaji bora wa Mashindano hayo.

Wakati yanatajwa majina matatu ya wachezaji wanaowania tuzo ya mchezaji bora wa FIFA wa dunia (Ballon d'Or) kipindi hicho,jina la kiungo Wesley Sneijder halikuwemo kwenye orodha hiyo,yaan wali-mupa Xavi waka-muruka Sneijder,waka-mupa Iniesta na KUMUPA tuzo hiyo Lionel Messi.

Baada ya hapo tuzo ikawa inahama kwa mtindo wa upatu,yaan nipe nikupe kati ya Messi na Ronaldo,inatoka Madrid inaenda Madeira kusalimia,ikitoka huko inarudi tena Hispania kwenye jimbo la Katalunya na kuelekea Rosario kupiga " selfie" na washkaji,hakuna upinzani.

Siku zikapita,ikawa mchana ikawa asubuhi,majira yakasogea,Uholanzi wakapotea kwenye Ulimwengu wa soka,Sneijder akatangaza kung'atuka kwenye soka la kimataifa,akatuachia mrithi wa kazi yake,naye ni Mtakatifu machoni pa wanandinga wengi duniani,Luka Modric wa Real Madrid na timu ya taifa ya Croatia.

Luca Modric akiipigania jezi ya Croatia

Mchezaji wa nafasi ya kiungo.
Nafasi aliyokuwa anacheza Sneijder wakati yupo Madrid ndio nafasi anayocheza Modric leo hii,namba ya jezi aliyoshinda nayo UEFA Sneijder ndio namba ya jezi aliyoshinda nayo Modric na kumpa tuzo ya mchezaji bora wa dunia.

Mafanikio ya timu zao za taifa kati ya wawili hao kwenye kombe la dunia yote ni sawa,wote walishika nafasi ya pili,japokuwa Modric alimaliza na magoli mawili lakini Sneijder alimaliza na magoli matano na hakupata tuzo yoyote,FIFA walimruka....MUPE,MURUKE,MUPEE,MURUKEE,MURUKEEE........!!!!

Huko alipo najua Sneijder anafurahia tuzo ya Modric,anajihisi ni kama ameipata yeye,kwani vigezo vilivyompa tuzo Modric ndivyo hivyo hivyo vilivyomnyima Sneijder,ama kweli dunia haina usawa...!!

Luca Modric akiwa kibaruani na jezi ya Real Madrid

Kitu pekee cha kujivunia kwa Sneijder ni ile huduma ya "free delivery" ya mipira aliyokuwa anaifanya uwanjani,sasa imepata mrithi sahihi ambaye ni Luka Modric na kutambuliwa mchango wake,anakupa akitaka,anakuruka asipotaka,na anafunga kwa mateso makali kama alivyomning'iniza Willy Caballero wa Argentina kwenye kombe la dunia.

@Sir_Rwechu
©2018

No comments:

Post a Comment

CAF kumuunga mkono INFANTINO Urais wa FIFA

Shirikisho la soka barani Afrika CAF linamuunga mkono Infantino Rais wa shirikisho la soka barani Africa (CAF) AHMAD AHMAD amesema shir...