![]() |
John Bocco mchezaji wa kwanza kufunga mabao 100 kwenye ligi kuu Tanzania bara |
Imebaki historia ya masimulizi ya mdomo,labda kama nikihitaji uthibitisho wa picha na maandishi,nitapita kwenye akaunti ya Instagram au Facebook ya Iddi Pazzy "father".
Atanipa masimulizi jinsi alivyouweka mpira kwapani na kuwakimbia watani zake wa jadi Yanga,atanisimulia jinsi Abdallah Kibadeni " King Mputa" alivyopiga hat-trick kwenye "Kariakoo Derby", atanionesha picha za kocha mzungu aliyewapa ubingwa " Wanalizombe",Majimaji ya Songea,Dimitry Samsalov,lakini sitopata takwimu za uhakika na video za kila mchezaji.
Ni rahisi kumfahamu Sir Matt Busby aliyeipa heshima Manchester United au Bill Shankly wa Liverpool kuliko kumchambua Sekilojo Chambua wa Yanga aliyestaafu soka juzi tu hapa wakati Tanzania ikiongozwa na Rais Benjamin William Mkapa.
Pengine majina ya Joseph Kaniki Golota na Emmanuel Gabriel Mwakyusa "Batistuta" yasiwe mageni masikioni mwa mashabiki wa soka,lakini walichokifanya katika enzi zao hakifahamiki kinaga ubaga.
Kumbukumbu nzuri inaweza kubaki kwa Shekhan Rashid jinsi alivyokuwa anawapigisha mbizi waarabu wa Misri,Al-Ismailia pale shamba la bibi lakini rekodi pekee inayomuhusu yeye utaipata Radio Tanzania Dar es Salaam (RTD-siku hizi TBC Taifa),jinsi mtangazaji alivyokuwa analitaja jina lake na kutangaza magoli na si vinginevyo.
Japokuwa kulikuwa na vipaji lukuki kwenye michezo mbalimbali ikiwemo na mpira wa miguu,lakini dhana duni za matumizi ya sayansi (teknolojia) zilitunyima uhondo wa kuwarithisha vizazi vyetu yale tuliyoyashuhudia kwa macho yetu.
Maendeleo ya matumizi ya sayansi yanayomtukuza John Raphael Bocco kuwa mchezaji wa kwanza kufunga magoli 100 katika ligi kuu ya soka ya Tanzania Bara,na kuanzia hapa ndipo tunapoanza kupata shujaa wetu wa mpira wa miguu.
Bocco anapitishwa kwenye kipindi cha kumbukumbu ya muda mrefu kutokana na takwimu zake kutunzwa vyema mitandaoni.Hivyo anakuwa bora kwenye takwimu mbele ya Sunday Manara "kompyuta", Zamoyoni Mogella,Peter Tino na wachezaji wengine waliong'ara kipindi hicho.
Sina haja ya kumtafuta Jaffar Iddi Maganga anisimulie au kunikabidhi makabrasha ya takwimu za Bocco,wala sitamtafuta John Raphael mwenyewe anipe masimulizi ya mdomo,nitaingia mtandaoni,nitaandika jina lake na kupata kila kitu cha kwake,Raphael+Technology+Era yaan RAPHAELOGY ERA....!!!
Tangu anatoka Kijitonyama FC,anatua Azam,anaipandisha timu na kucheza ligi kuu kwa mara ya kwanza mwaka 2007,Bocco takwimu zake zipo.
![]() |
John Bocco akiwa kwenye jezi ya Azam FC ambayo aliifungia magoli 84 kwenye ligi kuu ndani ya misimu tisa |
Tunampata Bocco mitandaoni akiitumikia timu ya Taifa ya Tanzania (Taifa Stars) kwa mara ya kwanza chini ya Marcio Basilio Maximo,amefanikiwa kucheza mechi 65 na kufunga magoli 16 mpaka sasa,huku hana rekodi za kutisha.
Ila ukija kwa upande wa ligi kuu,hakuna anayeweza kumpata Bocco kutokana na uwezo wake wa kufumania nyavu,magoli 100 ndani ya misimu kumi akiwa na Simba na Azam,sio kazi rahisi.
Pengine bahati yake njema kuchezea klabu kama Azam, klabu inayojiendesha kisasa zaidi kwa kuweka kumbukumbu sawa sawia za kila mtumishi wake,yaan wachezaji mpaka wataalam wa benchi la ufundi.
Huenda kama angeanzia soka lake klabu ya Simba kisha kuelekea Azam,labda hata yeye mwenyewe asingejua kama amefikisha magoli 100.
Nina uhakika kuwa kuanzia sasa na kuendelea,si Bocco tu lakini hata Kevin Pius John wa Serengeti Boys atatunziwa kumbukumbu zake vyema kutokana na maendeleo ya matumizi ya sayansi,yaan teknolojia.
Hata kadi nyekundu aliyoipata jana dhidi ya Mwadui ya Shinyanga kwa kumpiga ngumi mlinzi Revocatus Richard,utaikuta kwenye mtandao hata ipite miaka elfu moja.
Kupitia kipindi hiki cha teknolojia ya hali ya juu,hakuna mchezaji ayakayeweza kudanganya umri,hata Bocco mwenyewe naamini ana miaka 29.
![]() |
John Bocco akiitumikia Simba Sc ambayo ameifungia magoli 16 mpaka sasa kwenye ligi kuu |
Teknolojia inanifahamisha kuwa Bocco amezaliwa August 5,1989,na mimi naamini Kwa kupitia teknolojia pia Bocco ataweza kupata timu yoyote nje ya Tanzania,akiwa kama mchezaji au mkufunzi kama atahitaji kufanya hivyo hapo baadaye,ni kwa sababu takwimu zake zipo na hazidanganyi.
Na kwa kupitia teknolojia,itawapa changamoto wafumania nyavu wengi hususani wanaochipukia kutaka kuvunja rekodi ya mkongwe huyu.
Nikiwa kama mdau wa mpira wa miguu,natoa pongezi za dhati kwa John Raphael Bocco "Adebayor" kwa kufikisha magoli mia moja (100) ya ligi kuu ya soka Tanzania Bara.
Bado bendera nusu mlingoti,tuendelee kuwaombea marehemu wote waliotangulia kwenye pumziko la milele,Mwenyezi Mungu awarehemu ndugu zetu.AMEN.
@Sir_Rwechu
©2018
No comments:
Post a Comment